Monday , 16th Sep , 2019

Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro linamshikilia mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Philipina Silayo, mkazi wa Kijiji cha Kitangara Wilayani Rombo kwa tuhuma za kumuua kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni mwanaye wa miaka mitano.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Hamis Issah

Inaelezwa kuwa mara baada ya kutekeleza unyama huo, aliamua kujisalimisha polisi kwa kuwapa taarifa za tukio lake alilotekeleza, ambapo polisi hawakuamini taarifa hizo hadi walipoenda kuhakikisha nyumbani kwake.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Hamis Issah amesema kuwa, tukio hilo lilitokea siku ya Septemba 15 na kwamba kwa taarifa za awali wamebaini kuwa Mwanamke huyo alikuwa na matatizo ya akili na Jeshi hilo linaendelea kumshikilia kwa mahojiano zaidi.

''Mwanamke huyo baada ya kufanya mauaji ya mwanaye, alijisalimisha mwenyewe kwenye kituo cha polisi cha Mashati na Polisi walipofika nyumbani kwake walikuta mwili wa mtoto huyo ukiwa chini chumbani, huku pembeni mwa mwili huo kukiwa na kisu cha matumizi ya nyumbani kikiwa na damu na awali ndugu na majirani walidai mwanamke huyo alikuwa na matatizo ya akili", amesema Kamanda Issah.

Kamanda Issah amesema kuwa, mwili wa Mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Huruma kwa ajili ya taratibu za mazishi.