Thursday , 5th Sep , 2019

Serikali ya Tanzania imesema kuwa,  itasitisha kwa muda safari za Ndege yake aina ya Airbus A22O - 300,  iliyokuwa inashikiliwa nchini Afrika Kusini kwa amri ya Mahakama ambapo jana iliachiwa,  kufuatia hali ya vurugu na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Ndege za Air Tanzania

Hayo yamebainishwa leo Septemba 05, 2019  na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe,  wakati wa Uzinduzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA).

''Kwa mujibu wa ratiba, kesho Ndege yetu  ilikuwa inatakiwa  iruke kurudi Afrika ya Kusini,  lakini ninyi ni mashahidi kwamba nchi ile kuna fujo kubwa inaendelea, kwahiyo tumeona kwamba hatuwezi kuwapeleka abiria eneo ambalo tunajua maisha yao yako hatarini, tunaomba muendelee kuvuta subra'' amesema Waziri Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe ameongeza kuwa,  safari hizo zitasitishwa hadi Serikali itakapofanya mawasIliano na Serikali ya Afrika ya Kusini ili kuhakikisha kwamba unakuwepo usalama wa chombo na  abiria waliobebwa na safari hizo zitarudi tena,  endapo watapokea barua ya kuwahakikishia ulinzi wawapo nchini humo bila madhara yoyote.