Friday , 2nd Aug , 2019

Jeshi la Polisi nchini limezuia safari za saa 24 za mabasi kwa baadhi ya mikoa kwa sababu ya kiusalama na kuwataka wamiliki wa mabasi hayo kuzingatia maagizo yaliyotolewa ili kulinda usalama wa wananchi.

Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 2 na Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo, Liberatus Sabas ambapo amesema licha ya kuruhusu  mabasi yote nchini kutembea usiku bila kulala sehemu yoyote, Jeshi la polisi limebaini kuna baadhi ya maeneo zoezi hilo limebidi lisubiri kidogo ili wajipange kwa ajili ya usalama na watakapojiridhisha safari hizo zitaendelea kama kawaida.

''Maeneo hayo ambayo tumeona yasubiri ni  yale mabasi yanayotoka Dar es Salaam kupitia Kahama kwenda Kigoma, itabidi yalale Kahama, na yale mabasi yanayotoka Dsm -  katavi - Kigoma kupitia Tabaora yalale Tabora, Dsm kwenda Kagera yalalae Kahama na kesho yake yaendelee na safari kwa sababu hizo hizo za kiusalama na yale mabasi yanayoanzisha Tabora kwenda safari za mbali yalale Tabora'', amesema Kamanda Sabas.

Mapema mwaka 2018, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alihoji kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro sababu inayopelekea mabasi yasisafirishe abiria hata nyakati za usiku, ambapo baadae aliagiza mabasi yote nchi yaanze kusafiri usiku na mchana.