Monday , 24th Jun , 2019

Kocha wa zamani wa Barcelona, Bayern Munich na Manchester United, Louis van Gaal amesema kuwa wachezaji nyota, Lionel Messi na Neymar sio wachezaji wa kucheza kitimu.

Messi na Neymar

Van Gaal, ambaye aliifundisha Barcelona kutoka 1997 hadi 2000 na 2002 hadi 2003, anaamini kwamba nyota hao wawili wanapaswa kuwajibika kutokana na lawama hizo.

"Iangalie Barcelona. Ni mara ngapi wameshinda kombe la Klabu Bingwa Ulaya wakiwa na mchezaji wanayemuita kuwa ni bora zaidi duniani?", aliiambia El Pais.

"Neymar naye akiwa na PSG. Ni mara ngapi wameshinda Klabu Bingwa Ulaya. Mimi nawapenda Neymar na Messi kama wachezaji binafsi lakini si kama wachezaji wa kitimu. Naamini kwamba katika michezo ya timu, hakuna kitu muhimu zaidi kuliko kucheza kitimu".

"Moja ya wachezaji bora ni James Milner, katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa, alicheza kama mlinzi na kama kiungo. Ni nzuri kwamba anaweza kuhudumu kazi  hiyo katika umri wa miaka 33", ameongeza.

"Nadhani Messi anapaswa kujiuliza haraka iwezekanavyo kwamba hajashinda Ligi ya Mabingwa kwa muda mrefu. Nampenda Messi kama mchezaji binafsi. Kwa sasa yeye ni mchezaji bora zaidi duniani kwa sababu takwimu zake ni za ajabu lakini kwanini hakushinda Ligi ya Mabingwa tangu miaka mitano iliyopita?, kwanini?. Kama nahodha lazima ujiulize kwa nini.

"Barca ina kikosi kizuri sana. Huwezi kusema kwamba Rakitic ni mbaya, au kwamba Coutinho ni mbaya, au kwamba Alba ni mchezaji mbaya, au Ter Stegen ni goalie mbaya, au Arthur au Vidal".

"Nadhani Messi pia anahusika na kinachotokea Barcelona - sio kocha tu. Wachezaji wana sehemu kubwa ya wajibu wa kile kinachofanyika kwenye timu hiyo."

Van Gaal amemalizia kwa kusema kuwa Guardiola aliifundisha Barcelona kwa mafanikio lakini makocha wa hivi karibuni wameshindwa kufanya hivyo, wamesalia kumtumaini Messi pekee badala ya kulinda roho ya timu, kitu ambacho ni muhimu zaidi.