Madini ya dhahabu
Akizungumza katika mahojiano maalum na Idara ya Habari Maelezo, Bungeni Jijini Dodoma, Waziri Biteko amesema kuwa kuanzishwa kwa masoko hayo kumekuwa chachu ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika kukuza uchumi na pato la Taifa kwa ujumla.
“Katika kipindi cha mwezi mmoja tu yaani Machi 17 mpaka Aprili 17 mwaka huu, jumla ya kilo 409.3 za dhahabu pekee zenye thamani ya shiilingi bilioni 34.3 zimeuzwa kupitia katika maduka yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali”, amesema Biteko.
“Katika kilo hizo, Mkoa wa Geita umeongoza kwa kufanya biashara ya jumla ya kilo 289, Kahama kilo 44, Mara kilo 13, lakini cha kufurahisha zaidi ni kwa Wilaya ya Chunya ambako jumla ya kilo 52 zimeuzwa katika soko hilo zikiwa ni siku chache toka kufunguliwa kwake”, ameongeza mheshimiwa Biteko.
Aidha mheshimiwa Biteko, katika mahojiano hayo maalum ameeleza kuridhishwa na biashara inayofanyika katika maduka hayo ya madini kote nchini na kueleza kuwa licha ya mafanikio hayo yaliyofikiwa katika kipindi kifupi, serikali inashughulikia changamoto ndogondogo ikiwemo wafanyakazi, mashine za XRF na idadi ya watoa vibali.
Pia aliwataka wachimbaji wadogo na madalali wa madini kuhakikisha kuwa wanatumia masoko hayo kikamilifu na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni jambo alilosema serikali haipendi.
Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Waziri Biteko amebainisha kuwa masoko mengine 7 yanatarajiwa kufunguliwa. Baadhi ya Mikoa ambayo imeshafungua masoko ya kuuza madini ni pamoja na Geita, Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, ambapo tayari mikoa 21 imeshafungua maduka hayo hadi sasa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli alilolitoa kwa wakuu wa mikoa wote nchini.