
Obrey Chirwa
Ameyasema hayo baada ya kuifunga Yanga mabao mawili katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi linaloendelea visiwani Zanzibar.
Chirwa amesema kuwa hakushangilia pindi alipoifunga Yanga kwasababu ya heshima kwa klabu hiyo lakini akisisitiza kuwa nia yake ni kuifunga Yanga na Simba iliyo na kikosi kamili, ili ajipime ubora wake dhidi yao.
"Nilipofunga magoli mawili sikushangilia kwasababu mimi naiheshimu Yanga, klabu ambayo imenilea kwa misimu miwili. Lakini ninatamani kuifunga Yanga na hata Simba ambayo ina kikosi kamili ili nione ubora wangu dhidi yao," amesema.
Aidha, Chirwa amesema kuwa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu bado ziko wazi kwa timu zote tatu, Yanga, Simba na Azam FC na yeye kama mchezaji, jukumu lake ni kuipigania timu yake iweze kushinda ubingwa huo.
Azam FC inaongoza kundi A katika michuano ya Mapinduzi, ikiwa na jumla ya alama nne, ikifuatiwa na Yanga yenye alama tatu. Pia ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo ikiwa imeshinda mara mbili mfululizo.