Mkuu wa Kurugenzi ya sheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo - Chadema, Tundu Lissu.
Mkuu wa kurugenzi ya sheria ya CHADEMA na msemaji wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni Tundu Lissu amesema hayo leo jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya chama hicho kutoa taarifa ya kuwepo njama za kutaka kukidhoofisha chama hicho.
Kwa mujibu wa Lissu, mamlaka ya nidhamu kwa wanachama wenye hadhi ya ubunge ni kamati kuu, chombo ambacho amesema ndiyo kilichotoa maagizo ya kwamba wajumbe wote wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA kutoka CHADEMA wasihudhurie vikao vya bunge maalumu la Katiba.
Wakati huo huo, hospitali na Vituo vya afya vya umma nchini Tanzania bado vinakabiliwa na tatizo sugu la uhaba mkubwa wa damu, kutokana na mwamko mdogo wa uchangiaji damu kwa hiari, kwa ajili ya kusaidia wagonjwa na watu wenye uhitaji.
Afisa uhamasishaji kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki Bi. Fatma Mjungu amesema hayo leo katika kambi maalumu ya kuchangia damu iliyopo barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, kambi iliyowekwa kwa msaada wa kliniki ya uchunguzi na tiba ya hospitali ya TMJ ya jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa hospitali ya TMJ Bi. Jenny Ocheng amewataka Watanzania kujitolea kuchangia damu kwa hiari ili kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wakiwemo akina mama wajawazito na wahanga wa ajali na kwamba katika kambi hiyo wanatarajia kukusanya chupa mia moja na hamsini za damu.