Wednesday , 7th Nov , 2018

Shujaa wa klabu ya Red Star Belgrade, Milan Pavkov ametoboa siri nzito baada ya kuifunga mabao mawili Liverpool katika mchezo wa klabu bingwa barani Ulaya usiku wa jana.

Milan Pavkov

Pavkov (24) ambaye alifunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 katika uwanja wake wa nyumbani amesema atakosa usingizi kwa muda wa siku tatu kutokana na ndoto yake kutimia.

"Nilikuwa nategemea hili kutokea, nilisema mwanzo kuwa ninataka kuja kuifunga Liverpool na ndoto yangu sasa imetimia na nimefunga mabao mawili", amesema Pavkov.

"Kuhusu kulala?, siwezi, siwezi kulala baada ya michezo kadhaa lakini sasa ni kwa mchezo mmoja tu. Sitoweza kulala kwa siku mbili au tatu", ameongeza mshambuliaji huyo.

Baada ya Liverpool kupoteza mchezo wa jana, inazidi kujiweka katika nafasi ngumu zaidi katika kundi C, ikiwa na alama 6 sawa na Napoli huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na PSG yenye alama 5. Red Star Belgrade yenyewe baada ya ushindi wa jana inasogea hadi katika alama nne, ikiwa ya mwisho katika kundi hilo.

Pia matokeo ya mchezo huo yameweka rekodi mpya kwa Red Star Belgrade ya kupata ushindi wa kwanza dhidi ya klabu kubwa katika michuano ya Ulaya tangu 1992 huku Liverpool ikilazimishwa rekodi ya kufungwa mabao 2-0 katika kipindi cha kwanza kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014 ilipofungwa katika mchezo wa klabu bingwa dhidi ya Real Madrid.