Sunday , 7th Oct , 2018

Mama mzazi wa aliyekuwa msanii wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba Florah Mtegoa amefunguka kuwa hana chuki na msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) na ikitokea akapata mualiko wa kuhudhuria harusi yake atakwenda japo mwanadada huyo ana mababa wengi.

Mama Kanumba amefunguka hayo katika mahojiano maalum na www.eatv.tv ambapo amesema kuwa endapo familia itaona ana umuhimu wa kufika atakwenda japo inaonekana hana vigezo wa kile alichodai kuwa mwanadada huyo ana baba zaidi ya mmoja.

Mama Kaumba alipoulizwa kuhusiana na kauli ya Lulu kuwa na Baba wengi alikataa kufafanua na kusisitiza kuwa utaelewa baadae, "Unajua Kanumba alikuwa na baba mmoja tu, Charles na Mungu wake lakini Lulu ana ma baba wengi na kama wakiniona nna kidhi vigezo vya kuhudhuria harusi yake nitakwenda", amesema Mama Kanumba.

Mama Kanumba ameongeza kuwa, "Hapa Duniani sina chuki na Lulu kabisa nina mtakia kila la kheri awe na amani kabisa, kwa sasa akili yangu ni moja tu kumuomba Mungu maana ndio mwenye haki sawa kwake hakuna tajiri wala maskini".

Septemba 30, muigizaji Elizabeth Michael (Lulu) ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha nje baada ya kukutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake Steven Kanumba, alivishwa pete ya uchumba na mpenzi wake wa muda mrefu, Francis Siza (Majizo).