Friday , 31st Aug , 2018

Klabu ya Coastal Union imetamba kuendeleza wimbi lao la ushindi dhidi KMC katika mchezo ujao wa ligi kuu Tanzania bara kutokana na historia nzuri waliyonayo dhidi yao katika ligi daraja la kwanza.

Mchezaji wa Coastal Union Alikiba

Akizungumza na www.eatv.tv kuhusu maandalizi kwa ujumla ya mchezo ujao wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya KMC, afisa habari wa klabu hiyo, Hafidh Kido  amesema.

“ KMC hawajawahi kuwa washindani wetu tangu tukiwa tunakutana nao katika ligi daraja la kwanza na hata katika mechi za majaribio, kwasababu KMC ni miongoni mwa timu changa sana nchini. Unapoizungumzia Coastal Union ni timu ambayo mwaka huu tunatimiza miaka 70 tangu ianzishwe, kwahiyo KMC ni timu ambayo sisi wala haitusumbui kwa lolote na sidhani kama watakuja kutufunga “.

Aidha, Hafidh Kido amezungumzi kuhusu suala la Alikiba kujiunga na kambi ya timu na uwezekano wa kuanza katika kikosi cha kwanza cha Coastal Union katika mchezo huo, ambapo amesema.

“ Kuna vitu watu wanachanganya, Alikiba ni mchezaji kama wachezaji wengine na ana hadhi sawa na wachezaji wengine, tofauti yake ni kwamba yeye ni mtu maarufu, kwahiyo yeye yupo kambini na anafanya mazoezi kama kawaida na suala la kucheza au kutocheza katika mchezo huo ni jukumu la mwalimu “.

Coastal Union inashika nafasi ya nne na alama zake nne mpaka sasa katika msimamo wa ligi baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare mechi moja huku KMC ikiwa na alama mbili baada ya kwenda sare michezo yake miwili.

Mchezo huo wa tatu mfululizo wa nyumbani wa Coastal Union katika ligi kuu msimu huu unatarajia kuchezwa Jumamosi, Septemba mosi katika dimba la Mkwakwani mkoani Tanga.