Sehemu ya nyavu haramu zikiteketezwa kwa moto
Serikali kupitia idara ya  uvuvi mkoani  mara  imeendesha  oparesheni  kali  na kufanikiwa kukamata  zana haramu  ambazo zilikuwa zikitumika  kuvulia  samaki  katika  ziwa  Victoria  zenye  thamani  ya  zaidi  ya  milioni Tisini  kisha  kuziteketeza  kwa  moto.
 
Akizungumza  wakati  wa  kuteketeza  zana  hizo  haramu  za  uvuvi  katika  zoezi  ambalo limefanyika  nje kidogo  ya  mji  wa  musoma, kaimu afisa  mfawidhi  doria  na udhibiti  wa  uvuvi kanda ya mara  Bw Alli Mzee Said, amesema jumla  ya zana haramu  11,397  zimekamatwa  katika opareshini  hiyo.
 
Amesema  katika  oparesheni hiyo ambayo imedumu kwa siku 21  na kuhusisha wilaya za Rorya, Butiama na Bunda, jumla ya  makokoro  ya  dagaa  na  samaki  aina  ya  sangara 155 na kamba zake za kuvulia kokoro mita 39,205 zimekamatwa  pamoja  na  nyavu 11,242 ambazo  haziruhusiwi  kisheria kuvulia   samaki pia zimekamatwa. 
 
Kwa upande wake kaimu mkuu wa wilaya ya musoma Bw John Henjewele, akizungumza baada ya kuwasha moto kwa ajili ya kuteketeza zana hizo haramu, amesema serikali haina nia ya kuwafilisi wavuvi na wafanyabiashara wa nyavu, bali wanapaswa kuzingatia sheria na kwamba  zoezi hilo linakuwa endelevu katika kupambana na uvuvi haramu katika ziwa Victoria.
Nao baadhi ya wakazi wa mkoa wa mara Bw David Katikiro na Bw Emmanuel Bwimbo, pamoja na kuipongeza serikali kwa jinsi inavyopambana na uvuvi haramu katika ziwa Victoria, lakini pia wamesema kuna haja kwa serikali kuchukua hatua ya kudhibiti uingizaji wa zana hizo kutoka nje ya nchi, hatua ambayo wamesema itasaidia kupambana na uvuvi huo haramu

