Rais Jakaya Kikwete, waziri mkuu wa Canada Stephen Harper na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon katika mkutano na wanahabari Toronto Canada
Tanzania imefanikiwa kufanikisha lengo la kupunguza vifo vya watoto kama yalivyoainishwa na Umoja wa Mataifa kwa juhudi za Serikali, familia na jamii kwa ujumla , ikiwa ni pamoja na msaada mkubwa kutoka kwa Jumuiya ya kimataifa, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na Mashariki binafsi mbalimbali ya kimataifa.
Rais Kikwete amesema hayo tarehe 29 Mei,2014 alipotoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano kuhusu afya ya Mama na Mtoto unaofanyika mjini Toronto, Canada.
Katika jitihada hizo Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga ambapo kuamkia milenia vifo vya watoto vilikuwa 115 kwa 1,000 na vya watoto wachanga chini ya miaka mitano vilikuwa 191 kwa 1,000. Kufikia sasa, vifo hivyo vya watoto wachanga vimefikia watoto 21 kwa 1,000 na watoto chini ya miaka mitano vifo vimepungua hadi kufikia 54 kwa 1,000.
Rais pia ameelezea kuwa utumiaji wa dawa za uzazi (contraceptives) umeongezeka kwa asilimia 27 kutoka asilimia 7 na wanawake wanaojifungua kwenye vituo vya afya na kusaidiwa na wakunga wenye ujuzi wamefikia asilimia 54 na matumizi ya chanjo kwa watoto yameongezeka.
Mambo mengine yaliyochangia katika kufanikisha, ni udhibiti na mapambano dhidi ya malaria na Ukimwi kama ilivoainishwa katika Malengo ya Milenia, ambalo ni lengo la 6, kuboresha lishe kwa watoto na kuwanyonyesha.
Ni dhahiri pia kwamba Serikali imeweka sera nzuri za Afya na kuboresha huduma za Afya na Uzazi Tanzania, kuongeza bajeti ya Afya kutoka shilingi 271 bilioni kwa Mwaka 2007 hadi shilingi trillion 1.4 kwa Mwaka 2013.
Katika hili serikali imejenga Zahanati 1,640, Vituo vya Afya 122 na Hospitali mpya 19. Pamoja na hayo, Hospitali za Mikoa na Wilaya , pamoja na Hospitali kubwa nchini ya Muhimbili zimeboreshwa.
Serikali pia imepandisha viwango Zahanati na Vituo vya Afya kadhaa ili kuweza kutoa huduma ya ukunga, kuongeza mafunzo kwa watumishi na pia kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa muhimu katika Afya.
Rais Kikwete ameuambia mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Canada Mhe. Stephen Harper, Malkia Rania wa Jordan na Bibi Melinda Gates wa Bill and Melinda Gates Foundation kuwa, ataongeza bajeti ya Afya na kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, washirika wa Maendeleo, na sekta binafsi na ana matumaini kuwa malengo haya yanaweza kuendelezwa na kufikiwa zaidi.
Mapema Waziri Mkuu wa Canada ametangaza msaada wa dola bilioni 3.5 katika kusaidia na kuboresha Afya ya Mama na Mtoto kwa kipindi cha Miaka 2015-2020 ambapo msaada mkubwa unalenga katika harakati za kupunguza vifo vya Mama na Mtoto hasa katika kuimarisha mifumo ya Afya, kuimarisha Lishe na kupunguza magonjwa na kuimarisha chanjo.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Ban Ki Moon amempongeza Rais Kikwete kwa jitihada zake za kulinda na kuleta Amani DRC Congo
"Napenda kutambua na kukushukuru kwa juhudi zako za kuunga mkono jitihada za Amani na Usalama DRC na kwingineko, natumaini utaendelea kutoa mchango wako na natazamia mchango wako mkubwa katika nchi za Maziwa Makuu" Mhe. Ban Ki Moon amemuambia Rais Kikwete ambaye naye ameahidi kutoa ushirikiano zaidi.