Wednesday , 21st May , 2014

Waandaaji wa pambano la masumbwi ya kuwania ubingwa wa kimataifa wa UBO uzito wa Super Middle kat

Anthony Luta (katikati) akiwa na mkanda utakaopiganiwa na Kalama Nyilawila(kushoto) na Said Mbelwa(kulia)

Waandaaji wa pambano la masumbwi ya kuwania ubingwa wa kimataifa wa UBO uzito wa Super Middle kati ya Kalama Nyilawila na Said Mbelwa, wamesema maadalizi yamekwisha kamilika kwa kiasi kikubwa na kilichobaki ni masuala madogo madogo ambayo yatakamilika kadri siku zinavyosogea.

Akiozungumza EATV wakati akitambulisha mkanda utakaopiganiwa, katibu mkuu wa PST ambao ndiyo wasimamizi wa pambano hilo bwana Anthony Luta amesema pambano hilo litakutanisha mabondia wenye sifa tofauti.

Luta amemtaja Kalama Nyilawila kama bondia pekee aliyekwenda Ulaya(pasipo msaidizi) na akafanikiwa kushinda ubingwa wa dunia pia akamtaja Said Mbelwa kama bondia wa kwanza kupigana nchini Afghanstan baada ya utawala wa Taliban na ndiye bondia aliyepigana mapambano mengi Ulaya.

Awali pambano hilo lilikuwa limkutanishe bondia Kalama Nyilawila na Thomas Mashali lakini Thomas Mashali akapata ajali ya gari iliyomsababishia majeraha makubwa na kupelekea Kalama Nyilawila abadilishiwe mpinzani ambaye kwa sasa ni Said Mbelwa.

Lakini Kalama mwenyewe anasema hiyo ilikuwa janja ya Mashali kumkwepa kwani hakupata ajali bali aliungua moto sehemu ndogo tu ya mwili wake.

Wakati Nyilawila akimpiga kijembe Thomas Mashali, Said Mbwelwa amemtahadharisha Kalama kwamba atarajie upinzani mkali kutoka kwake kuliko ule ambao angeupata kutoka kwa Thomas Mashali.

Pambano hilo litafanyika Jumamosi hii katika ukumbi wa Friends Corner Manzese na kutakuwa na mapambano kadhaa ya utangulizi likiwemo la mwanamuziki Halid Choraa atakayepigana na Mabondia Abdul Banyenza katika pambano la Raundi nane uzito wa kilo 60 yaani Light Weight.