Friday , 16th Dec , 2016

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini imetoa vitabu vipya vya kiada kwa elimu ya msingi na sekodari ambayo itatumika katika mtaala mpya wenye maudhui yatakayomuwezesha mwanafunzi kuwa na ujuzi na uwezo wa kujitegemea mara baada ya kuhitimu.

Vitabu

 

Akiongea na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dk. Elia Kibga amesema vitabu hivi ni vya kwanza kuandikwa ili kukidhi mahitaji ya utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya ufundi ya mwaka 2014 na kwamba vitaanza kutumika mapema mwezi Februari mwaka 2017 kwa shule za Tanzania Bara.

"Vitabu 6 vya elimu ya awali vimeandikwa na viko katika hatua ya kutafuta wazabuni wa kuchapa, vitabu 5 vya darasa la kwanza vimekamilika na tayari vinatumika, vitabu 6 vya darasa la pili vimekamilika na viko katika hatua ya uchapaji katika makampuni mbalimbali"

Dk. Elia amesema, mbali na kutoa vitabu hivyo pia wanalenga kuhakikisha kuwa tatizo la uhaba wa vitabu vya kiada na kufundishia katika shule zote za sekondari na msingi litakuwa historia ifikapo mwezi Machi mwaka 2017 na kwamba wataondoa changamoto ya uwepo wa vitabu tofauti tofauti kwa somo moja ili wanafunzi wote nchini wajifunze na kupimwa kupitia kitabu kimoja.

Kuhusu vitabu vinavyotumika katika shule zinazotumia Kiingereza, amesema "Taasisi ya Elimu Tanzania pia imeandaa vitabu 15 vya masomo kwa shule zinazotumia lugha ya kiingereza katika kufundisha na kujifunza kwa darasa la I-III. Vitabu hivyo vipo katika hatua ya usanifu na vitakuwa tayari mwishoni mwa mwezi Machi, 2017"