Tuesday , 22nd Nov , 2016

Tanzania imekuwa ikinufaikia na fursa za kiuchumi na kibiashara zilizomo ndani ya soko la pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki licha ya changamoto ndogo zinazohitaji ufuatiliaji ili kuboresha ushiriki wa wafanyabiashara wa Tanzania katika soko hilo.

Louis Accaro

 

Mkuu wa Huduma za Wateja kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi nchini TPSF Bw. Louis Accaro, amesema hayo leo wakati wa mkutano wa wadau, ulioandaliwa na TPSF kwa ajili ya kupata tathmini ya sasa ya ushiriki wa Tanzania katika soko hilo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kila mdau wa soko hilo.

Washiriki wakubwa katika soko hilo ni wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo ambapo katika maelezo yake, Mwenyekiti wa Vikundi vya Wafanyabiashara Ndogondogo VIBINDO SOCIETY Bw. Gaston Kikuwi ametaja tozo kubwa kutoka kwa wakala mbalimbali za serikali kuwa ni kikwazo cha wao kushiriki katika soko hilo.

Kwa upande wake, Afisa kutoka Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda Bw. Octavian Kivyiro amesema serikali mara zote itahakikisha maslahi ya kiuchumi ya Tanzania katika soko hilo yanalindwa.