Monday , 14th Nov , 2016

Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, hii leo imesikiliza kwa mara ya pili kesi yake ya kwanza inayowakabili watanzania wawili na raia mmoja wa China.

 

Kesi hiyo ya kwanza katika mahakama hiyo imesikilizwa kwa mara ya pili leo, ikiwakabili watu watatu akiwemo raia mmoja wa China, Fu Chang Feng, na watanzania wawili ambao ni Jeremia Madar Kerenge na Ally Danji Lazer wakishtakiwa kwa kosa la kuingiza bidhaa zilizokatazwa za uvuvi katika Bahari Kuu zenye dhamani ya Shilingi Bilioni 7 na Milioni 485 za Tanzania.

Wakili wa upande wa utetezi Roman Ramwai ameiomba mahakama hiyo kuwapatia dhamana watuhumiwa wawili raia wa Tanzania, Ombi ambalo Jaji Rehema Mkuye wa mahakama hiyo italitolea uamuzi tarehe 16 Mwezi huu baada ya Wakili wa serikali mkuu Wakili Timon Vitali kusema kuwa upande wa Jamuhuri hauna pingamizi dhidi ya dhamana hiyo na kwamba mahakama inaweza kuwapatia dhamana watuhumiwa hao.

Akiongea na EATV mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Charles Magesa ameelezea aina mbalimbali ya kesi ambazo mahakama hiyo ina uwezo wa kuzisikiliza na kwamba mahakama hiyo itatumia muda mfupi sana hadi kutolewa hukumu tofauti na mahakama nyingine.