Thursday , 27th Oct , 2016

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeamua kushusha chini zaidi madaraka kwa wanachama wake katika ngazi ya familia kwa njia ya kuanzisha mabalozi wa nyumba kumi kama ilivyo kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Dkt. Vincent Mashinji

 

Akijibu maswali ya wananchi kupitia KIKAANGONI ya Facebook.com/eatv.tv, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Vincent Mashinji amesema kuwa chama hicho hivi sasa kimeamua kuzidi kujiimarisha katika ngazi ya familia, hivyo kugatua madaraka kutoka juu, kwenda katika ngazi ya kanda hadi mabalozi wa nyumba kumi.

Amesema hatua hiyo itarahisisha watu kukifahamu zaidi chama hicho pamoja na sera zake, pia itakuwa rahisi kutoa elimu ya uraia kuanzia ngazi ya familia, lakini pia itawawezesha viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya chini kuwa na uwezo wa kushughulikia harakati pamoja na matatizo yatakayokuwa yakijitokeza, na hatimaye kukiwezesha kushika dola katika uchaguzi wa mwaka 2020.

"Tayari tumekwishafanya uzinduzi wa mpango wa mabalozi wa nyumba 10 katika wilaya ya Kinondoni, na tumesimika mabalozi katika kata ya Mwananyamala Dar es Salaam kama sehemu ya kuanzia. Mpango huu utafanyika nchi nzima, na kila balozi atakuwa na jukumu la kujenga chama katika ngazi ya familia" Amesema Dkt. Mashinji.

Ameongezea kwa kusema kuwa  hivi sasa chama hicho kinafanya kazi kwa mikutano ya ndani, ambapo viongozi wote wakuu wa chama watapita kwenye kanda zote kufanya ukaguzi na ufuatiliaji, ili kuhakikiksha chama hicho kinakuwa na wanachama wapya, watakaokiwezesha kushinda katika kila uchaguzi.

KIKAANGONI ni programu ambayo hufanyika mubashara kila Jumatano saa 8 mchana hadi saa 10 jioni kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV, ambapo watu mbalimbali hupata nafasi ya kujibu maswali ya wananchi.