Monday , 27th Jun , 2016

Timu ya Taifa ya Tenisi Walemavu imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa mashindano ya wazi ya Tenisi walemavu Jijini Nairobi nchini Kenya.

Kocha wa timu hiyo Riziki Salum amesema, wamewakuta wapinzani wao wakiwa wamejipanga vizuri kwa ajili ya mashindano hayo lakini kwa kuwa walikuwa na lengo la kutetea ubingwa waliweza kupambana na kutimiza lengo walilojiwekea.

Riziki amesema, licha ya mazingira magumu katika maandalizi pamoja na ushiriki wao kiujumla lakini waliweza kupambana na changamoto hizo na kuweza kuutetea ushindi ambao waliweza kuutwaa hapo mwaka jana.

Riziki amesema, aliondoka na kikosi cha wachezaji 11 ambao sita kati yao walikuwa ni wachezaji chipukizi ambao waliweza kujitahidi japo hawakuweza kuchukua ushindi katika mashindano hayo.

Riziki amewataka wadau mbalimbali wa michezo nchini kuweza kujitokeza kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo ambayo inahitaji viti vya matairi vya walemavu kwa ajili ya kuweza kupata urahisi watakaposhiriki mashindano mengine.