Monday , 20th Jun , 2016

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimestushwa na kufadhaishwa na maamuzi yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kutangazwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari bila ya kufuata misingi ya Katiba na Kanuni.

Jengo la ofisi za makao makuu ya TFF Dar es Salaam.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kupitia KATIBA na KANUNI za TFF, DRFA, na KIFA kimejiridhisha kwamba maamuzi yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya kufuta matokeo halali ya uchaguzi wa Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni uliofanyika siku ya Jumapili tarehe 12/06/2016 katika bwalo la maofisa wa polisi Oysterbay bila hayakuzingatia katiba na kanuni za TFF, DRFA na KIFA.

Maamuzi hayo ya TFF yamevunja katiba ya TFF, DRFA na KIFA pamoja na kanuni zake ambazo ndiyo mwongozo wa mpira wetu hasa katika upatikanaji wa mamlaka za uendeshaji wa mpira katika ngazi mbalimbali za taifa, mkoa na wilaya.

Katiba ya TFF ibara ya 52(2) na ibara ya 52(6)(a) zinaeleza wazi kazi na majukumu ya kamati ya uchaguzi ya TFF ni kwa chaguzi za TFF na wanachama wake ambao ni vyama vya mikoa, vilabu vya ligi kuu na kusimamia uchaguzi wa Board ya ligi pamoja na kuishauri kamati ya utendaji mambo yanayo husiana na chaguzi hizo.

Kwa mujibu wa katiba ya TFF ya 2013 kamati yake ya uchaguzi haiwajibiki na lolote kwa vyama vya mpira wa miguu vya wilaya ambao si wanachama wa TFF. Lakini pia Ibara ya 3(i) ya kanuni za uchaguzi za TFF za 2013 inaeleza kuwa kamati ya uchaguzi ya TFF itaendesha na kusimamia uchaguzi wa TFF na Bodi ya Ligi.

Ibara ya 6 ya kanuni za uchaguzi za TFF za 2013 pia inaeleza majukumu ya kamati ya uchaguzi na katika majukumu yake hakuna popote inapoonyesha kuwa ina mamlaka ya kusimamia na kutolea maamuzi chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya wilaya ambao si wanachama wa TFF.

Kwa mujibu wa Katiba ya KIFA ibara ya 47 na kanuni za uchaguzi kipengele (b) inasema Kamati ya Uchaguzi ya KIFA itafanya kazi kwa kushirikiana na sekretarieti ya Chama na chini ya uangalizi na Miongozo ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA. Kwahiyo ni jukumu la kamati ya uchaguzi ya DRFA kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kugundua kwamba Kamati yake ya Uchaguzi haina mamlaka ya KIKATIBA kuweza kusimamia chaguzi za vyama vya wilaya, miongoni mwa mapendekezo ya mabadiliko ya katiba waliyoleta katika Mkutano Mkuu wa TFF wa mwisho uliofanyika Tanga ni pamoja na hilo kuuomba mkutano mkuu wa TFF uweze kufanya hilo badiliko ili waweze kusimamia chaguzi za WILAYAwilaya lakini bahati mbaya marekebisho ya katiba hayakuweza kupitishwa na wajumbe wa mkutano.

Katiba ya KIFA katika kanuni zake za uchaguzi 5 (h) inatamka kwamba rufaa zote zihusuzo uchaguzi zitawasilishwa kwenye kamati ya rufaa ya Wilaya na hatimae kama Mrufani hakuridhika basi atakata rufaa katika kamati ya rufaa ya Mkoa ambapo uamuzi wake utakuwa ndio wa mwisho.

Baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya KIFA kutangaza matokeo ya uchaguzi huo tajwa hapo juu na kutuletea ripoti yake, mmoja wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti Bwana Thomas Mazanda aliamua kukata rufaa katika Kamati ya uchaguzi ya Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kama katiba ya KIFA inavyoelekeza kupinga matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi wa KIFA.

Lakini cha kushangaza wakati kamati ya uchaguzi ya DRFA ikipanga kusikiliza rufaa hiyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likaitisha kikao 18/06/2016 na kuamua kufuta uchaguzi huo bila kufuata taratibu za kikatiba na kikanuni zinazotuongoza.

Kamati ya Uchaguzi ya Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni kwa mujibu wa Ibara ya 47 inaundwa na wajumbe watano. Wajumbe wa kamati hii watateuliwa na Mwenyekiti. Na Mwenyekiti wa kamati hii lazima awe ni mwanasheria na wajumbe wengine wane lazima wawe ni watu wenye ujuzi na upeo katika masuala ya michezo.

Kwa mujibu wa katiba ya KIFA haina makamu mwenyekiti wala katibu wa kamati. Na maadam katiba inatamka wazi Mwenyekiti lazima awe mwanasheria tafsiri yake ni kwamba bila uwepo wa Mwenyekiti kamati haiwezi kuendelea na kazi zake kwa sababu ukiondoa Mwenyekiti wajumbe wengine waliobaki wa kamati ya KIFA hawana taaluma ya sheria.

Katika kuakikisha uchaguzi huo wa KIFA una kuwa huru na haki Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya KIFA alialika watu tofauti tofauti kuhudhuriailia katika uchaguzi huo wakiwemo mwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa SPUTANZA Taifa na Mjumbe Mmoja wa Kamati ya Utendaji ya TFF katika uchaguzi huo.

Kwa mlolongo huu wa matukio ni dhahiri TFF imepora mamlaka ya kamati ya uchaguzi ya KIFA na DRFA kwa kuingilia na kufuta uchaguzi wa KIFA ambaye kikatiba ni mwanachama wa DRFA. Lakini pia TFF hii imefanya maamuzi yanayofanana na hayo katika uchaguzi wa Chama Cha Mpira Miguu Wilaya ya Temeke.

Uporaji huu wa madaraka ya mwanachama wa TFF ni hatari, batili na kinyume cha utaratibu tuliojiwekea hivyo kufanya hata maamuzi hayo yaliyofanywa na TFF kuwa batili. Hii inatokana na ukweli kuwa kutokana na katiba zetu TFF haina nguvu yoyote ya kikatiba wala kikanuni ya kutolea maamuzi mchakato wa uchaguzi wa chama cha wilaya ambaye ni mwanachama wa chama cha mpira wa miguu cha mkoa.

kwa haya yanayoendelea katika TFF ni dhahiri kuwa taasisi hiyo sasa inaondokana na utaratibu wa kuendesha mambo yake kwa kuegemea misingi ya KATIBA na KANUNI zake na badala yake kuendesha mambo yake ki – imla. Ni jambo la hatari kwa taasisi kubwa kama TFF kuendesha mambo yake ki – imla kwani itapoteza heshima iliyojijengea kwa miaka mingi.