
Madereva wa magari ya abiria maarufu kama daladala yanayofanya safari zake kutokea kituo cha Mawasiliano kwenda Makumbusho kupitia chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamesitisha shughuli ya kusafirisha abiria kwa muda kufuatia kile wanachodai kuwa ni madereva Bajaji kuwaingilia kwenye njia zao.
Akiongea na East Afriaca Radio katibu wa madereva hao Bw Deogratius Mlowo amesema kuwa uwepo wa Bajaji hizo zinabeba abiria tena kwa bei sawa na daladala kumedhoofisha sana biashara yao na baadhi ya madereva kushindwa kufikisha kiasi cha pesa walichotakiwa kulipa kwa mabosi zao.
Aidha walishatoa taarifa kwa viongozi wanaohusika bila ya mafanikio yoyote huku wakipewa ahadi kuwa watu wa sumatra watakuja kufanya upembuzi ili waweze kutatua tatizo hilo lakini mpaka sasa tatizo hilo limeshindwa kushughulikiwa.
Kwa upande wake mmoja kati ya madereva wa daladala hizo amesema kuwa wanaitaka serikali iwape ufafanuzi ni nani anaetakiwa kutumia njia hiyo kati ya daladala au bajaji.
