Wednesday , 8th Jun , 2016

Beki Mkongo mwenye uwezo wa kucheza nafasi za kiungo Mbuyu Junior Twite ameongeza Mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Yanga huku kiungo kutoka Niger Issoufou Boubacar Garba amepewa barua ya kuvunjiwa Mkataba.

Kiungo Mniger Issoufou Boubacar kulia akiwa na Mkuu wa kitengo cha habari na mahusiano cha Klabu ya Yanga Jerry Muro

Garba ameachwa kwa sababu ya kushindwa kuwa katika kiwango kinachohitajika kwa matumizi ya timu hiyo, wakati Mbuyu kwa mara nyingine akijivunia matunda ya kazi yake awapo uwanjani.

Garba alisajiliwa na Yanga SC Desemba mwaka jana baada ya majaribio ya siku mbili tu, lakini tangu hapo amecheza mechi 11 na kufunga mabao matatu likiwemo lile la katika sare ya 1-1 na Al Ahly ya Misri mjini Dar es Salaam katika Ligi ya Mabingwa Afrika miezi miwili iliyopita.

Kabla ya kutua Klabu ya Yanga Garba amewahi kuchezea AS FAN na AS Douanes zote za kwao Niger, Muangthong United na Phuket za Thailand, Club Africain na ES Hammam-Sousse za Tunisia.