Friday , 3rd Jun , 2016

Timu ya taifa ya Misri kesho inatarajia kuumana na Taifa Stars katika mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), lakini taarifa za ubora wa nahodha wa Stars, Mbwana Samatta zimekuwa zikikivuruga kikosi hicho.

Taifa Stars yenye pointi moja itapambana na Misri yenye pointi nne katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ikihitaji matokeo ya ushindi kwa ajili ya kujiweka katika mazingira mazuri.

Ingawa katika mchezo wa kwanza Mafarao hao walifanikiwa kuifunga Stars ikiwa ugenini mabao 3-0, lakini bado wamekuwa na wasiwasi kulingana na kiwango cha Stars na hasa Samatta anayeonekana kung’ara akiwa na timu yake mpya ya KRC Genk ya Ubelgiji, akiwa ameshaifungia mabao matano hadi sasa.

Katika mazoezi yao walikuwa wakiulizia taarifa za Samatta kuhusu ujio wake kila wakati na kutaka kujua kama kuna baadhi ya wachezaji wenye kiwango kama chake ambao hawajasikika lakini wapo Stars.

"Vipi Samatta amekuja? Tunamfahamu yule tangu yupo TP Mazembe (DR Congo), tunajua kiwango chake na ndiyo ambaye tunajua atatusumbua," waliulizia Wamsiri.

Samatta amejiunga na Stars iliyo chini ya Kocha Boniface Mkwasa jana akitokea Ubelgiji wakati Thomas Ulimwengu anayekipiga Mazembe yeye alishatua tangu juzi, tayari kwa mechi hiyo.