Friday , 27th May , 2016

Serikali imesema kuwa itaufanyia marekebisho ya haraka mfumo wa utoaji risiti na changamoto nyingine katika mradi wa mabasi yaendayo haraka(U-DART),ili mradi huo utoe tija ya haraka kama inavyohitajika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ndani ya basi la Mradi wa Mabasi yaendayo haraka UDART.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mradi huo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa zipo changamoto ambazo ameziona mara baada ya ziara hiyo ambazo serikali itazifanyia kazi ili kuboresha zaidi usafiri huo.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amewataka watumishi wa mradi huo kufuata sheria ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wananchi ambao wameonekana sio waaminifu kwa kufanya udanganyifu wa kurejea vituo na tiketi za siku iliyopita.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema baada ya mradi huo kuboreshwa zaidi itakua haina ulazima wa watu kwenda na magari yao mpaka mjini hivyo watatakiwa kupaki nje ya mji na kutumia usafiri huo kuelekeza kwenye shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani, Mohammed Mpinga, amewataka watumiaji wa barabara kufuata sheria na kuacha kuzitumia njia hizo na endapo mtu akikiuka adhabau kali itachukuliwa dhidi yake.

Aidha, Kamanda Mpinga ameongeza kuwa jeshi la Polisi na Kikosi cha usalama barabarani wataendelea kutoa elimu kwa Wananchi watembea kwa miguu ili waelewe matumizo ya barabara hizo ikiemo kutumia vivuko pindi wakitaka kuvuka barabara.

Sauti ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa