Waziri wa kushughulikia Majanga na Masuala ya Wakimbizi wa Rwanda Seraphine Mukantabana.
Waziri wa kushughulikia Majanga na Masuala ya Wakimbizi wa Rwanda Seraphine Mukantabana amesema kutimuliwa huko kwa raia wa Burundi ni sehemu ya msako wa kawaida wa wanaoishi kinyume na sheria nchini Rwanda na sio msako wa kuwalenga hususan Waburundi.
Uhusiano kati ya nchi hizo jirani umekuwa ukizorota. Msako huo wa Rwanda unafuatia wa Burundi uliopelekea maelfu ya Wanyarwanda kufukuzwa tangu mwezi Aprili mwaka jana.
Burundi imekuwa katika mzozo wa kisiasa tangu mwaka jana baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kugombea muhula wa tatu madarakani na kuchochea maandamano na ghasia ambazo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 500 na kusababisha wengine 250,000 kuyatoroka makazi yao.
Burundi inaishutumu Rwanda kwa kuwafadhili waasi wanaotaka kumng'oa madarakani Nkurunziza, madai ambayo Rwanda imeyakanusha vikali.