Sunday , 15th May , 2016

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI nchini Tanzania, Mhe. Suleiman Jaffo, amewataka wasimamizi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (UDART) kuharakisha uimarishaji wa mfumo wa ulipaji nauli kwa kutumia kadi za kielektroniki.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI nchini Tanzania, Mhe. Suleiman Jaffo.

Akizungumza leo wakati akitembelea mradi huo eneo la Kimara Mwisho, Jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaffo amesema mfumo wa kadi utarahisha ulipaji na utatumia muda mfupi ukilinganisha na tiketi, huku akiwataka wananchi kuvitunza vituo pamoja na kufuata taratibu zilizowekwa pindi wanapotumia usafiri wa mabasi hayo.

Mhe. Jaffo ametembelea vituo hivyo ambapo leo ndio siku ya mwisho ya abiria kusafiri bure kwa ajili ya kupewa elimu juu ya usafiri huo kabla ya hapo kesho kuanza rasmi kutozwa nauli iliyotangazwa na serikali kwa ajili ya usafiri huo.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa Tanzania imekua nchi ya kupigiwa mfano katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo daraja la Kigamboni hivyo kuanza kwa mradi huo kutaiongezea sifa Tanzania kwa kupiga hatua za kimaendeleo.