Viongozi wa juu wa Baraza la Michezo nchini Tanzania BMT.
Baraza la michezo nchini Tanzania BMT limekabidhi majukumu ya moja kwa moja kwa shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kuhusiana na uchaguzi wa klabu ya soka ya Yanga na kulitaka shirikisho hilo kuhakikisha suala hilo linafikia tamati ifikapo June 30 mwaka huu.
Kaimu katibu mkuu wa BMT Mohamed Kiganja amesema uamuzi huo umetokana na klabu ya Yanga kutokuwa na viongozi wakuchaguliwa kwa mujibu katiba na kisheria ambao kwa hali iliyopo sasa hauna mamlaka tena ya kuteua kamati ya uchaguzi. kama kifungu F cha katiba ya Yanga kinavyoelekeza [ ibara ya 45] na hivyo anaagiza mambo yafuatayo yafanyike kwa mujibu wa sheria ya kuundwa kwa Baraza la Michezo Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni za Baraza na Kanuni za Msajili namba 442 za mwaka 1999 -:
{1} Uchaguzi wa Yanga ufanyike na mchakato wake uanze wiki hii na mwisho wa mwezi Juni mwaka huu, Uongozi mpya wa Yanga uwe madarakani [huku Baraza kazi yake ni kuhakikisha hawavunji katiba za wadau wao].
{2} Katiba itakayotumika ni ile ya mwaka 2010 na watakaoingia madarakani wataingiza vipengele vya mabadiliko ndani ya Katiba ya Yanga kama ambavyo Mdau wao Mkuu TFF atakavyowaelekeza.
{3} Kadi za Wanachama wa Yanga katika uchaguzi huo zitatumika zile zilizowahi kutumika chaguzi zilizopita na zenye saini za ya mwenyekiti wa klabu na katibu wa klabu na si zile kadi za taasisi za fedha [mabank] mahususi za wanachama na mashabiki kwaajili ya kuchangia mapato kwa timu hiyo.
{4} Na pia baraza linawaagiza TFF kusimamia Uchaguzi huo mara moja, na mikutano ya kuweka taratibu za uchaguzi zianze ndani ya wiki hii.
Aidha Baraza linawaagiza TFF kuhakikisha kuwa vilabu vyote vinavyoshiriki ligi kuu kufanya uchaguzi, kwani ni vilabu vitatu tuu mpaka sasa ndivyo vimekamilisha mchakato huo kwa mujibu wa katiba ambavyo ni Simba, Coastal Union na African Sports hivyo vilabu vilivyobaki vifanye chaguzi zao mara moja.
Na pia ameigiza TFF kwenye kanuni zake iweke sheria kali zinazotekeleaeka ili kudhibiti ujanja wa baadhi ya vilabu kukwepa kufanya uchaguzi.
Akimalizia Kiganja ameviagiza vyama na mashirikisho ya michezo yote nchini ambayo hayajafanya uchaguzi yafanye uchaguzi ili vilabu, vyama na mashirikisho hayo yatawaliwe kisheria na kwa mujibu wa taratibu za kikatiba.