Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dkt. Augustine Mahiga
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bw Augustine Mahiga ameelezea mbele ya Waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, na kusema kuwa kushtushwa kwake na hatua hiyo ya bodi ya MCC ni kutokana na kupuuza hatua kubwa tu zilizopigwa kidemokrasia nchini Tanzania.
Kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar Bw Mahiga anasema kuwa Tanzania, ilifanya kila kitu kuambatana na sheria na katiba ya nchi wala hakuna tatizo ama ukiukwaji wa sheria.
Mahiga anasema kuwa huo ni uamuzi wao na kwa sababu hela hizo ni zao wanauhuru wa kuzitumia watakavyo ila anahoji kwanini uamuzi huo uliafikia bila ya majadiliano na serikali ya muungano ya Tanzania.
Waziri huyo ameonya kuwa watu wanaoishi vijijini ndio watakaoathirika zaidi kwani fedha hizo zilikuwa zimepangiwa kueneza umeme mashinani.
Katika kutoa uamuzi wake, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ilisema kuwa Tanzania haijatimiza viwango vinavyohitajika ili kunufaika na ufadhili kutoka kwa shirika hilo, na hivyo basi haitapokea msaada wa awamu ya pili.