Mabula ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Hot Mix kinachorushwa na kituo cha EATV kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa, saa moja jioni.
"Meya kweli ametoka upinzani ila kuwa Meya wa jiji la Dar es salaam siyo kazi kubwa kwa sababu hata vyanzo vyake vya kukusanya mapato sii vingi hapa atakusanya zaidi kwenye 'packing' ya magari (ushuru wa maegesho)".
Mabula ameongeza kuwa cheo cha umeya wa Dar es salaam kimekaa kisiasa ndiyo maana hata alivyokuwepo Dkt. Didas Masaburi kazi yake ilikuwa ni kushiriki kwenye shughuli za kitaifa na kwenda kupokea wageni uwanja wa ndege wanaokuja kufanya ziara hapa nchini.
"Kwa Dar es salaam, kila kitu kiko chini ya manispaa, jiji halimiliki kitu, halimiliki shule, wala barabara na hata vyanzo vyote vya mapato vinamilikiwa na manispaa tatu ambazo ni Temeke, Ilala na Kinondoni, Meya wa jiji hana kauli yoyote kwa rasilimali karibu zote za maendeleo"
Mabula ambaye alikuwa Meya wa Jiji la Mwanza kabla ya kuchaguliwa na wananchi kuwa mbunge wa jimbo hilo amesema katika kipindi chake akiwa Meya, aliweza kutumia vizuri fedha za maendeleo kujenga barabara kutoka Mkuyuni kwenda Butimba kilomita 18 pamoja na kujenga tanki kubwa la maji eneo la Kishiri ambalo linahifadhi maji zaidi ya lita laki mbili pamoja kuelekeza fedha za serikali miradi mingine.
Aidha mbunge Mabula ambaye yupo katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ameeleza kusikitishwa kwake kwa baadhi ya kamati kuanza kukumbwa na kashfa za rushwa na kupelekea baadhi ya wabunge kujiuzulu na kusema kuwa hali hiyo haioneshi picha nzuri katika kuwatumikia wananchi.