Nyamweya ametoa tamko la kujitoa katikati ya shughuli ya upigaji kura mchana wa leo mbele ya wajumbe takriban 77 ambao ndiyo wapiga kura.
Wengine waliokuwepo wakati Nyamweya akitoa taarifa hiyo ni maofisa wa serikali akiwemo Katibu wa Baraza la mawaziri anayeshughulikia michezo Hassan Wario na maofisa wengine kutoka shirikisho la soka duniani FIFA.
Awali uchaguzi huo uliahirishwa mara tatu kutokana na sababu ambazo baadhi ya wadau wanadai kuwa hazikuwekwa bayana.
Uchaguzi wa leo ulikuwa na wagombea sita wa urais wa shirikisho lakini hadi majira ya mchana walikuwa wamebaki wagombea wawili pekee baada ya kujiondoa kwa Sam Nyamweya, ambaye ameongoza shirikisho hilo kwa miaka minne.
Wagombea wengine watatu, Sammy Shollei, Semi Aina na Semelang’o walijiondoa mapema.
Kujiondoa kwa wagombea hao kumeacha kinyang’anyiro sasa kuwa kati ya Nicholas Mwendwa na Ambrose Rachier.
Wadau wengi wa soka nchini humo wanataka mabadiliko ikikumbukwa kuwa mwaka jana, shutuma zilielekezwa kwa shirika hilo baada ya wachezaji wa timu ya taifa Harambee Stars kuchelewa kusafiri kwenda Cape Verde kwa ajili ya mechi ya marudio ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi..



