Wednesday , 9th Apr , 2014

Jeshi la polisi mkoa wa Mara nchini Tanzania kwa kushirikiana na raia wema limefanikiwa kuwakamata watu 22 kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kuwachinja na kuwanyonga wanawake saba kutoka baadhi ya vijiji vya mwambao wa Ziwa Victoria.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Ernest Mangu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Kamishina msaidizi mwandamizi Ferdinand Mtui amewaambia waandishi wa habari kuwa katika matukio hayo ya kikatili na kinyama watu 10 tayari wamefikishwa mahakamini huku wengine kumi na wawili wakingojea taratibu za kisheria ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hata hivyo kamanda Mtui ameomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha watu wote wanaohusika katika mtandao huo wa mauaji ya kikatili ya wanawake kwa imani za kishirikina, wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya kisheria, huku akisema tayari mbunge wa musoma vijijini ametoa ahadi ya shilingi milioni moja kwa kila mwananchi atakayelisadia jeshi la polisi kukomesha mauaji hayo.