Tuesday , 9th Feb , 2016

Mbunge wa jimbo la Mikumi, Joseph Haule (CHADEMA ) maarufu kama prof J amesema hali ya wananchi katika jimbo lake hususani wananchi wa kata ya Tindiga wilayani Kilosa ni mbaya sana kutokana na mafuriko kusomba nyumba zao zaidi ya 600.

Haule ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na EATV kuhusiana na hali ya wananchi wa jimbo lake ambao wamekumbwa na mafuriko na kusababisha zaidi ya kaya 5000 kukosa makazi na kuhifadiwa na ndugu zao huku wengi wakihama maeneo na wengi wakikosa pa kujihifadhi.

''Hali ni mbaya sana maji hayo yanatokana na mto Mpwapwa kupasuka kingo zake, pamoja na kupasuka kwa bwawa la Kidete baada ya kuzidiwa na maji hivyo maji hayo moja kwa moja yanafika kwenye makazi ya wananchi na kufanya wawe wahanga na kutafuta namna ya kujilinda''Amesema Prof. J

Haule ameongeza kuwa wanafunzi wamekwama kimasomo lakini pia huduma nyingine nazo ni ngumu kupatikana pia ugonjwa wa kipindupindu upo hatarini kuongeza kasi mkoani Morogoro kwa sababu baada ya mafuriko hayo wananchi nao wametapisha vyoo hivyo kipindupindu ni rahisi kulipuka.

Aidha mbunge huyo amesema yeye amepeleka msaada wa awali wa maji ya kunywa lita elfu 13 na anaomba msaada kwa serikali na yeyote mwenye mapenzi mema kuweza kujitolea mahema, chakula na dawa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hao.