Friday , 22nd Jan , 2016

Mgambo wa Manispaa ya Morogoro wakishirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na JWTZ wametumia nguvu kuwaondoa wafanyabiashara wa vyakula na matunda wanaofanya biashara hiyo pembezoni mwa barabara zikiwa ni jitihada za kutokomeza kipindupindu.

Mgambo wa Manispaa ya Morogoro wakiwakamata kwa nguvu baadhi ya Wananchi waliokaidi zoezi la kuondolewa kwa mama ntilie katikati ya Mji

Operesheni hiyo imekuja kufuatia mkoa wa Morogoro kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kipindupindu kati ya mikoa 10 inayokabiliwa na ugonjwa huo.

Baadhi ya wafanyabiashara na mashuhuda wa operesheni hiyo wameeleza kusikitishwa na zoezi lililofanywa na mgambo hao kwa wamewafanyia vitendo vya udhalilishaji kwa kuwapiga bila huruma na kwamba wangetumia utaratibu mwingie bila kuwabughudhi wafanyabiashara.

Wakizungumzia operesheni hiyo afisa afya manispaa ya Morogoro Bw. Gabriel Malisa na afisa tarafa Morogoro Bw. Pakapakara Mulenge wamesema operesheni hiyo inalenga kutokomeza ueneaji wa ugonjwa wa kipindupindu na kwamba zoezi hilo ni endelevu hadi ugonjwa huo utakapoisha.