Thursday , 21st Jan , 2016

Serikali imekanusha uvumi wa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa amefukuza wageni kutoka nje waliokuwa wanafanya biashara zao nchni kwa kuwa serikali yake haitaki wageni kufanya biashara nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Habari MAELEZO (katikati),Bi Zamaradi Kawawa akitoa ufafanuzi juu ya taarifa za uzushi unaosambazwa katika mitandao ya Kijamii ya ndani na nje ya nchi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimwa Dkt. John Pombe Magufuli amefukuza wageni kutoka nje waliokuwa wanafanya biashara hapa nchini

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema kuwa serikali haijafukuza wageni kutoka nje ya nchi kufanya biashara nchini na haina mpango wa kuwafukuza wageni wanaoishi nchini kwa vibali vilivyotolewa kisheria na Idara ya Uhamiaji.

Taarifa hiyo inasema kuwa Uzushi huo usiokuwa na ukweli umeenezwa kufuatia Idara ya Uhamiaji kutekeleza jukumu lake la kufuatilia wageni wote wanaoishi nchini bila vibali halali vya ukaazi ambapo kwa mwezi Novemba na Desemba mwaka 2015 wageni 372 walioondoshwa nchini.

Taarifa hiyo kutokaka ikulu imefafanua zaidi na kusema kuwa Uzushi unaoenezwa hauna nia njema na nchi kwani kati ya mwaka 2014 na 2016 Idara ya Uhamiaji imetoa vibali vya ukaazi (Residence Permits) 40,765 kwa wageni wawekezaji na wafanyabiashara, wageni wanaofanyakazi za kuajiriwa, wageni wanaokuja kwa ajili ya Masomo, matibabu, dini, utafiti na wastaafu kuishi na kufanya shughuli zao nchini.

Aidha taarifa hiyo kwa vyombo vya habari imesema kuwa Serikali inawakaribisha wageni kuja nchini kuwekeza na kufanya shughuli zao kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.

Kazi ya kufuatilia wageni wanaoishi nchini bila vibali halali vya kisheria haijaanza katika Serikali ya Awamu ya Tano. Idara ya Uhamiaji nchini tangu Januari hadi Desemba mwaka jana iliondosha nchini jumla ya wageni 1,642 waliokuwa wanaishi na kufanya shughuli zao nchini kinyume na Sheria.

Aidha, kuna uzushi unaenezwa kuwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amepiga marufuku wanawake kuvaa nguo fupi kama njia ya kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.

Mheshimiwa Rais tangu aingie madarakani hajawahi kuagiza wala kutoa tamko kuhusiana na uzushi wa kukataza uvaaji wa nguo fupi ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi kama inavyoenezwa katika mitandao ya ndani na Nje ya Nchi ambayo inanukuu habari hiyo kuwa imeandikwa na Gazeti la Kenya “The Standard”

Serikali inapenda kuutangazia umma kuwa uzushi huo unaomhusu Mheshimiwa Rais Magufuli umetungwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kwa lengo la kumdhalilisha Rais na hauna ukweli hivyo watu wasishiriki kuueneza kwa njia yeyote ile.

Serikali kupitia balozi zake za Kenya na Afrika Kusini zinafuatilia chanzo cha uzushi huu kuhusu Rais Magufuli kwa kushirikiana na nchi husika na watakaobainika kutunga na kueneza uzushi huu watachukuliwa hatua za kisheria.