Michuano ya nne ya kombe la Afrika kwa wachazaji wanaocheza ligi za ndani ijulikanayo kama CHAN kwa 2016 yataanza kutimua vumbi kesho nchini Rwanda.
Michuano hii ya Chan inashirikisha mataifa kumi na sita yatakayochuana kuwania ubingwa huo wa Afrika, huku Rwanda wakiwa wenyeji kwa mara yakwanza.
Viwanja vinne vitatumika katika michuano hiyo, ambavyo ni Uwanja wa Amahoro wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000 uliopo katika jiji la Kigali na uwanja wa Stade Huye uliopo katika mji wa Butare ukiwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000.
Uwanja mwingine utakatumika ni ule Regional Nyamirambo wa Kigali wenye uwezo wa kubeba watazamaji 22,000 na ule Umuganda ulioko Gisenyi ukichukua washabiki wa soka wapatao 5,000.
Wenyeji Rwanda wako kundi A wakiwa na mataifa ya Gabon, Morocco, Ivory Coast watatumia viwanja vya Amahoro na Stade Huye.
Kundi B lina timu za DR Congo, Angola, Cameroon na Ethiopia na zitatumia viwanja vya Amahoro na ule wa Stade Huye.
Katika kundi C kuna timu za Tunisia , Nigeria, Niger na Guinea ambazo zitachuana katika viwanja vya Regional Nyamirambo na ule wa Umuganda.
Timu za Zimbabwe Mali Uganda pamoja na Zambia wao wako kundi D, ambapo zitatumia viwanja vya Umuganda na Regional.
Michuano hii itafikia tamati Februari 7 kwa mchezo wa fainali itakaopigwa kwenye dimba la Amahoro Jijini Kigali.