Monday , 28th Dec , 2015

Kamati ya ulinzi na usalama mkoani Morogoro imesitisha rasmi zoezi la ubomoaji wa nyumba lililokuwa likifanyika katika eneo la CCT Forest kata ya Mkundi katika manispaa hiyo baada ya kuibuka hali ya sintofahamu kwa baadhi ya nyumba kubomolewa.

Diwani wa kata ya Mkundi Hilda Benedict

Wakizungumza na wananchi wa eneo hilo baada ya kutangazwa rasmi na serikali kusitishwa kwa zoezi hilo, mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdulaziz Abood amesema hawatakuwa tayari kuona kiongozi yeyote wa serikali anasababisha migogoro kama iliyojitokeza katika eneo la hilo kwakuwa imesababisha hasara na usumbufu mkubwa na kimewafanya wananchi kupoteza imani na serikali yao.

Mh. Abood ameongeza kuwa hawatamvumilia mtu yeyote atakayerudisha migogoro ya aina hiyo huku diwani wa kata ya Mkundi Hilda Benedict akiwasihi wananchi kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki wakati wakishughulikia maswala ya malipo ya fidia kwa nyumba 15 zilizokwishavunjwa.