Monday , 21st Dec , 2015

Tofauti na wa wasanii wengi kudai kwamba hakuna ulazima wa msanii kutoa albam, msanii wa muziki wa bongo fleva Mwana FA, amesema kutoa albam kwa msanii ni kitu cha lazima.

Mwana FA ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kuwa kuna haja ya wasanii kujipanga na kufikiria ni jinsi gani watauza albam hiyo.

"Kufanyika albam ni lazima lakini tuje na idea ni jinsi gani tutauza, tunaweza kuifanya hii kazi ya distribution wenyewe, au tunaweza kuwafikia wale watu ambao wahindi hawawafikii, ninachofikiri si tumekwama, hatukuwa na invest ment kwenye muziki au hatujafungua vichwa vyetu", alisema Mwana FA.

Pia Mwana FA amesema kipindi cha nyuma wasanii walikuwa wanatoa albam tofauti na sasa, na kwamba wasanii wenye uwezo wa kutoa albam ni wachache wenye kuhesabika.

"Si tulianza muziki kipindi ambacho hatukuwa tunaamini kwamba muziki utatuingizia hata elfu kumi, sasa hivi hatuna wasanii wengi wa kutoa albam wanahesabika", alisema Mwana FA.