
nembo ya shirikisho la soka nchini TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limevitaka vilabu vyote nchini vya Ligi Kuu ,Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kuheshimu utaratibu uliowekwa wa usajili na utekelezaji wake, kwani TFF haitapendelea klabu yoyote katika suala hilo.
Katika taarifa yake shirikisho hilo limesema linawakumbusha viongozi wote wa vilabu kuhusu kalenda ya mwaka ya usajili ambayo ina vipindi viwili cha kwanza ni Dirisha Kubwa la Usajili Juni 15 hadi Agosti 20 na Dirisha Dogo ni Novemba 15 hadi Disemba 15.
Baada ya usajili hufuatia kipindi cha pingamizi ambacho kuchukua wiki moja, kisha Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF kupitia mapingamizi hayo na kupitisha usajili wa wachezaji wote waliosajiliwa.
Kipindi cha usajili wa dirisha dogo ulifunguliwa Novemba 15 na utafungwa leo Disemba 15, ambapo kipindi hiki hutumika kwa ajili ya uhamisho, kutangaza wachezaji wanaoachwa kwa mujibu wa kanuni, kutangaza wachezaji waliositishiwa mikataba, na kipindi cha pingamizi Disemba 16 – 22, na kuthibitisha usajili Disemba 23, mwaka huu.