
Ofisi ya msajili wa vyama vya michezo Tanzania, imekiagiza chama cha mchezo wa kuogelea Tanzania TSA kutengeneza katiba mpya mara moja ndani ya siku 90.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hii leo, Afisa Habari wa Baraza la Michezo Tanzania BMT Najaha Bakari amesema maagizo hayo yalitolewa mara baada ya uchaguzi wa kupata viongozi wapya wa chama hicho waliochaguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye uchaguzi uliofanyika mkoani Morogoro.
Najaha amesema katiba ya sasa inawanyima haki baadhi ya wajumbe kupiga kura, hali iliyoleta malalamiko kwenye uchaguzi huo, ambapo aliyekuwa katibu mkuu kwenye uongozi uliomaliza muda Noel Kihunsi alijitoa.
Viongozi wapya waliochaguliwa kuongoza chama cha mchezo wa kuogelea Tanzania TSA ni Alex Mushi (Mwenyekiti),Paulia Hassan Dilia (Makamu Mwenyekiti) na Ramadhani Mkoveke (Katibu Mkuu).