
Rai hiyo imetolewa na msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva) Rama dee alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari, kuhusiana na changamoto za kilimo, na nini serikali ijayo ifanye ili kuweza wavutia vijana kujiingiza kwenye kilimo.
Rama dee amesema ingawa hapa nchini kuna vyuo vikubwa vinavyotoa taaluma ya kilimo, lakini watu hawaamini kama wanaweza kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo.
"Vyuo vipo vya kilimo, ila watu hawaoni kama kusomea kilimo unaweza kujikwamua kimaisha kama kusomea sheria n.k, lakini hii inatokana na serikali kutoelimisha jamii sawa sawa", alisema Rama Dee.
Rama Dee ambaye kwa sasa yuko nchini Australia, amesema pia vijana wengi hawapendi kuchagua kazi za kilimo, kutokana na sekta hiyo kutopewa kipaumbele, na pia vijana wengi wanapenda kutumia njia za mkato katika maisha na kufanikiwa kwa haraka.
"Vijana wengi kwa sasa wanaamini wanaweza kufanikiwa kupitia njia za mkato, na pia imekuwa ngumu kijana kuchagua kazi za kilimo kutokana na sekta hii ipo kama haipo", alisema Rama Dee.
Pia Rama Dee ameiataka serikali kuboresha bei za mazao ili kuweza kuongeza ajira kwa vijana na kuinua pato la Taifa, na pia kutapunguza ongezeko la watu wanaokimbilia mjini.
"Watu wanatoka vijijini wanakuja mjini unafikiri kwa nini...!? Hakuna msaada wa kumfanya mkulima ajisikie mkulima,...Bei za kuuza na kununua ziboreshwe kwa wakulima hiii itasaidia sana kuongeza ajira kwa vijana na pato la Taifa", alisema Rama Dee.
Rama Dee hivi karibuni alisema kwa sasa anajihusisha na kilimo, na kwa kupitia kilimo ameajiri vijana wenzake kupitia ukurasa wake wa twitter.