Friday , 2nd Oct , 2015

Idadi ya wagonjwa wa saratani nchini Tanzania inaongezeka siku hadi siku hususani kwa wanawake ikielezwa kuwa hali hiyo inatokana na elimu iliyotolewa kwa wananchi hivyo wengi kujotokeza kupima afya zao.

Gloria Kida akizungumza na Mkurugenzi wa IAEA Yukiya Amano.

Hayo yamesemwa na Gloria Kida ambaye ni manusura wa saratani ya matiti na ameshiriki katika mkutano wa kimataifa kuhusu upatikanaji wa matibabu ya saratani kwenye nchi zenye kipato cha kati na cha chini uliofanyika hivi karibuni mjini Vienna, Austria, wakati wa kongamano la kila mwaka la IAEA.

Bi. Gloria amesema kuwa katika kipindi cha nyuma watu wengi walikuwa hawana elimu kuhusu ugonjwa wa saratani lakini baada ya elimu watu wengi wamekuwa wakijitokeza kwenda kupima Saratani.

Hata hivyo Gloria amebainisha kuwa changamoto kubwa inayojitokeza ni kupatikana kwa idadi kubwa ya wagonjwa ambapo kwa mwaka inakadiriwa kuwa na wagonjwa wanaofikia elfu 40 lakini wanaopata tiba ni wachache kutoka na gharama za matibabu ya Ugonjwa huo.

Aidha Bi. Gloria ameongeza kuwa IAEA imeunda mkakati uitwao PACT wenye lengo la kupunguza kwa theluthi moja idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa saratani kwa kipindi cha miaka kumi na tano ijayo katika nchi zinazoendelea, kupitia uhamasishaji wa jamii na upatikanaji wa vifaa vya vipimo na matibabu.