Klabu ya Yanga leo imewapa raha wapenzi na mashabiki wake hii leo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Amis Tambwe dakika ya 44 na Malimi Busungu dakika ya 79.
Katika mchezo huo ambao timu zote mbili zilionesha dhamira ya ushindi, Simba iliyotawala zaidi kipindi cha kwanza, ilishindwa kutumia nafasi kadhaa ilizoweza kutengeza ikiwemo ile aliyopata Said Ndemla dakika za mwisho huku Yanga wakiweza kutumia nafasi chache walizopata kukwamisha mipira miwili wavuni.
Golikipa wa Yanga Ally Mustapha Bahtez aliweza kuonesha kiwango cha hali ya juu kwa kupangua michomo kadhaa ya hatari kutoka kwa washambuliaji wa Simba wakiwemo Awadh Juma, Hamisi Kiiza na Mussa Hassan ‘Mgosi’
Katika mchezo huo pia, beki wa Yanga Mbuyu Twitte alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kupata kadi ya pili ya manjano dakika ya 90.
Kwa ushindi huu Yanga imelipiza kisasi kwani katika mchezo uliopita Simba ikiwa haipewi nafasi, iliweza kuishinda Yanga kwa bao 1-0 lililofungwa na Emmanuel Okwi.
Yanga sasa imefikisha pointi 12 ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja, huku Simba ikibaki na point zake 9 kwa kushinda mechi 3.
Katika mashamba ya miwa Manungu Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar imeendeleza wimbi lake la ushindi kwa kuichapa Majimaji ya Songea bao 1-0 likifungwa na Shiza Ramadhani Kichuya dakika ya 70 kwa mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa Majimaji kuunawa mpra katika eneo la hatari.
Mtibwa pia imefikisha point 12 sawa na Yanga ikiwa imeshinda mechi nne mfululizo.
Jijini Mbeya wajelajela timu ya Prisons ya Mbeya imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Mgambo, bao lililofungwa na Said Mkopi dakika ya 66 ya mchezo.
Matokeo ya mechi nyingine zilizopigwa leoni :-
Coastal Union 0-0 Mwadui
JKT Ruvu Stars 0-1 Stand United
Tanzania Prisons 1-0 JKT Mgambo
Mtibwa 1-0 Majimaji
Kagera Sugar 0-0 Toto Africa
Kesho ni:-
African Sports Vs Ndanda FC
Azam Fc Vs Mbeya City.