Fomu kwa ajili ya nafasi za kugombea uongozi wa chama cha kuogelea Tanzania TSA zimeanza kutolewa kwenye Baraza la michezo Tanzania BMT, na Baraza la michezo Zanzibar BMZ.
Afisa Habari wa BMT Najaha Bakari amesema,fomu hizo zimeanza kutolewa tangu Septemba 10 na mwisho wa kuchukua fomu hizo ni Septemba 30 mwaka huu,ambapo ametoa wito kwa wadau wa mchezo wa kuogelea kujitokeza kuchukua fomu hizo ili kuongoza chama hicho na kuleta maendeleo katika mchezo huo.
Amesema uchaguzi wa TSA unatarajiwa kufanyika Oktoba 10 mwaka huu Mkoani Morogoro, na nafasi zinazogombaniwa ni Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti, Katibu Mkuu na Msaidizi wake, Mweka hazina na msaidizi wake, pia kuna nafasi za ujumbe ambazo ni Mkurugenzi Mwakilishi wa makundi maalum, Mkurugunzi mwakilishi wa vilabu, Mkurugenzi wa ufundi, Mkurugenzi wa fedha na wajumbe wawili kutoka chama cha kuogelea visiwani Zanzibar.

