Friday , 25th Sep , 2015

Mgombea Urais kutoka chama cha TLP Macmillan Lyimo amesema wataondoa ubaguzi uliopo kati ya watoto wa maskini na wale wa viongozi na matajiri, ili waweze kupata elimu sawa, iwapo watafanikiwa kuchaguliwa kuingia madarakani

Macmillan Lyimo ameyasema hayo alipokuwa akichat moja kwa moja na mashabiki katika kipengele cha Kikaangoni Live, kinachoendeshwa na kituo cha televisheni cha East Africa Television (EATV) na East Africa Radio, kupitia mtandao wa Facebook.

Lyimo amesema sera ya elimu bora na bure kwa watoto wote inawezekana, kwa kuwa nchi ina rasilimali za kutosha, na kuondoa utofauti mkubwa uliopo kati ya watoto wa viongozi na wananchi wa kawaida.

Lyimo ambaye alikuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya TLP kabla ya kugombea urais, ameendelea kwa kusema kwamba nchi sasa inahitaji mabadiliko, hivyo Wanaandaa njia nya kumpata kiongozi wa wakulivusha Taifa.

KUHUSU KUJIUNGA NA UKAWA

Katika maelezo yake Bwana Macmillan Lyimo amesema hajakataa yeye kujiunga UKAWA, isipokuwa wakati inaanzishwa hakuwepo, hivyo endapo atafanikiwa kuingia madarakani, hilo ni moja ya mipango yake kwani nae anaamini katika mabadiliko.

“Sikuepo ilianza bungeni ila wakati ukifika hilo ni hitaji muhimu, muda muafaka ukifika linawezekana”, alisema Lyimo.

KUHUSU HALI YA KISIASA ILIVYO

Akiendelea kufanya mazungumzo na wananchi kupitia mtandao wa kijamii, Bwana Lyimo amesema hali ya kisiasa ilivyo hivi sasa ni ya kutupiana vijembe na si kutoa sera kwa wananchi, na kwamba yeye yuko tayari kwa mdahalo kwani wengi wanaonekana kuukimbia.

Bwana Lyimo alimaliza kwa kusema kwamba iwapo atafanikiwa kuingia madarakani, atautupa mwenge wa uhuru baharini, kwani ndiyo uliopelekea watu kuwa malofa.

“Nitatupa mwenge katikati ya bahari maana ni uchawi uliotufanya malofa, mtafunguka akili na hamtanisau daima.
Mwenge ndiyo uchawi wetu na mgombea wa CCM kaubeba juu ya jina lake, Ila kwisha habari yao”, alisema Lyimo.