Tuesday , 8th Sep , 2015

Wananchi nchini Tanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ili kuweza kuchanganua na kuchagua viongozi wenye nia ya dhati ya kuongoza taifa na sio kuchagua kwa ushabiki.

Mkurugenzi wa kituo cha haki za binadamu LHRC Dkt. Hellen Kijo Bisimba

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) Dkt Hellen Kijo Bisimba ambapo amesema ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika uchaguzi na kwa kutambua umuhimu huo wameandaa ilani inayotoa muongozo kuhusu umuhimu wa uchaguzi na kupiga kura.

Bisimba amesema katika ilani hiyo inatoa muongozo kwa viongozi wa nafasi mbalimbali kuwajibika kwa wananchi baada ya kutoa ahadi zao ikiwemo suala la upatikanaji wa katib,a mgawanyo wa madaraka, utawala wa sheria na ulinzi wa haki za binadamu na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za umma.

Hata hivyo Bisimba amesema matarajio makubwa kwao ni kwa wananchi kuchagua viongozi ambao wanaamini watawasaidia kuleta maendeleo pamoja na vyombo vya utetezi wa haki za binadamu na tume ya uchaguzi kusimamia zoezi zima la kampeni na hata uchaguzi ili kulinda amani ya nchi.

Awali katika uzinduzi wa ilani hiyo mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Tanzania Bw. Bahame Nyanduga aliwataka wagombea, vyama vya siasa na raia kujiepusha na matumizi ya lugha ya chuki uchochezi na ubaguzi ili kuepusha uwezekano wa kutokea machafuko katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

Bw. Nyanduga aliongeza kuwa uzinduzi wa Ilani hiyo umekuja wakati muafaka ambapo utasaidia kuweka muongozo wa uwajibikaji, usawa wa kijinsia na utekelezaji wa ahadi zilizowekwa pamoja na kukemea vitendo vya rushwa.