Monday , 24th Mar , 2014

Mbunge wa Tunduru mkoani Ruvuma nchini Tanzania, Mtutura Abdallah Mtutura, amesema pembe za ndovu zinazokamatwa jimboni kwake ni za tembo wanaouwawa katika mbuga ya Niasa nchini Msumbiji na si jimboni kwake kama ambavyo wengi wamekuwa wakidhania.

Mheshimiwa Mtutura amesema hayo leo katika mahojiano ambapo pia amekanusha taarifa za chombo kimoja cha habari kuwa yeye pamoja na baadhi ya wabunge wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ujangili.

Mtutura amesema licha ya kuwepo kwa msitu wa hifadhi wa Mwambesi jimbo lake limekuwa ni njia ya majangili na wawindaji haramu, ambao hutumia jiografia nzuri ya mawasiliano kupitisha shehena ya pembe za ndovu kutoka nchi jirani ya Msumbiji kuelekea Jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, ambako inadhaniwa ndiko kwenye soko zuri la pembe hizo.