Yanga ikijiandaa na Kagame chini ya kocha Pluijm
Akizungumza jijini Dar es salaam, Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye amesema mashindano hayo ambayo ni makubwa yatakayomalizika Agosti 2 yatashirikisha timu 13 ambapo watahakikisha yanakuwa mazuri kwani wanaamini timu zote zimejiandaa vizuri.
Musonye ameyataja makundi ya timu shiriki katika michuano hiyo ambapo Kundi A kuna timu za Yanga ya Tanzania, Gor Mahia ya Kenya, Khartoum FC ya Sudan, Telecom ya Somalia na KMKM ya Zanzibar.
Musonye amesema makundi mengine ni kundi B ambalo lina timu za APR ya Rwanda, Shandy ya Sudan, Lydia Ludic ya Burundi na Hegaan FC ya Somalia huku kundi C likiwa na Mabingwa wa mwaka jana, Azam FC wamepangwa Kundi C pamoja na Malakia ya Sudan Kusini, KCCA ya Uganda na Adama City ya Ethiopia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga, amesema, timu shiriki katika michuano hiyo zitatakiwa kujilipia huku CECAFA wakiendelea kuwalipia viongozi wake pamoja na wale watakaochezesha mechi hizo ambapo amewaomba mashabiki kujitokeza kwa ajili ya kutoa sapoti kwa timu shiriki za michuano hiyo.