Mkoa wa Mara umeanza zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR huku kasoro mbalimbali zikiripotiwa kujitokeza katika maeneo mbalimbali mkoa huo yakiwemo ya wilaya za Butiama na Musoma mjini baada ya mashine hizo kushindwa kufanya kazi kwa muda na kusabisha zoezi hilo kuchelewa kuanza na kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi.
Baadhi ya wananchi hao katika manispaa ya Musoma mkoani Mara, ambao wamefika katika vituo mbalimbali vya kujiandikisha kuanzia saa kumi alfajiri leo na kukuta msongamano mkubwa wa watu, wamesema maandalizi hafifu ambayo yamefanywa na tume ya taifa ya uchaguzi yamesababisha kutozifanyia majaribio mashine za uandikishaji kwa mfumo wa BVR na kusababisha baadhi ya vituo zoezi hilo kuchelewa.
Hata hivyo wananchi hao wameiomba tume ya taifa ya uchaguzi kurekebisha kasoro hizo ikiwa ni pamoja na kufikiria kuongeza muda wa kujiandikisha ili kuhakisha kila mtu anapata fursa ya kujiandikisha.
Kwa upande wake afisa uchaguzi wa manispaa ya Musoma Buhabi musiranga, amesema zoezi hilo limefanyika kwa hali ya amani na utulivu na kwamba kasoro ambazo zimejitokeza zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja kuweka chumba maalum kwa ajili ya wazee na watu wenye ulemavu.