Friday , 26th Feb , 2016

Klabu ya Yanga imesema itakuwa makini kwa wananchi wote wanaotumia mchezo wa kesho wa marudiano wa klabu bingwa Afrika kati yao na Cercle De Joachim ya nchini Mauritius kwa ajili ya kujinufaisha.

Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga, Jerry Muro amesema, kumekuwa na wananchi ambao wanatoa tiketi feki za mchezo huo na kuuzia mashabiki ikiwa ni sehemu ya kujinufaisha wao na kuihujumu klabu isiweze kupata mapato wanayoyatarajia katika mchezo wa kesho utakaofanyika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Muro amesema, wananchi wote wanatakiwa kuwa makini na tiketi watakazouziwa kwa ajili ya mchezo wa kesho kwani vimewekwa vituo maalumu na vituo vilivyowekwa awali kwa ajili ya uuzwaji wa tiketi hizo vimefungwa na hapo kesho tiketi zote zitapatikana uwanja wa Taifa katika vituo maalumu.

Muro amesema, wao kama wasimamizi wa mchezo huo watahakikisha wanasimamia uuzwaji wa tiketi kwa mashabiki kwa kupima na vifaa maalumu kwa ajili ya kuitambua tiketi ambazo ni feki.