Friday , 18th Dec , 2015

Vinara wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Yanga imemtambulisha nyota wake mpya wa kimataifa kutoka Niger mbele ya waandishi wa habari Boubacar Yusuph kwa kumkabidhi jezi namba 14 tayari kwa kuanza kuwatumikia wanajangwani hao.

Nyota mpya wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Yanga Boubacar Garba akiwa kwenye jezi ya timu yake ya Taifa ya Niger

Akimtambulisha nyota huyo mbele ya waandishi wa Habari mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu hiyo Jerry Muro amesema nyota huyo pamoja na Paul Nonga aliyesajiliwa akitokea Mwadui ya Shinyanga wamesaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Muro amesema lengo la usajili huo ni kuhakikisha wanaendeleza kufanya vyema kwenye ligi ya nyumbani na michuano ya Kimataifa.

Naye nyota huyo amesema amefurahi kutua Jangwani na kuomba sapoti kutoka kwa mashabiki na kuwaahidi kufanya vyema kwa kuwa anauzoefu wa michezo ya kimataifa ambao pia aliupata akiwa na timu yake ya Taifa kwenye fainali za mataifa ya Africa mwaka 2013 na ile ya mwaka jana.

Wakati huo huo kuhusu mechi yao ya kesho dhidi ya Stand united Jerry Muro amesema wamejipanga na tayari nyota wote waliokuwa majeruhi wameanza maozezi huenda wakatumika kwenye mechi hiyo.