Monday , 28th Dec , 2015

Klabu ya Yanga imevunja Mkataba na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kutokana na mchezaji huyo kukiuka vipengele.

Mkuu wa idara habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga Jerry Muro amesema licha ya kuachana kuvunja naye mkataba pia mchezaji huyo anatakiwa kuilipa klabu hiyo kiasi cha Dola za Kimarekani 71, 175 zaidi ya milioni 143 za kitanzania ikiwa ni kufidia gharama ambazo Yanga imezitumia katika kumuongezea mkataba wake mpya ambao ungemalizka mwaka 2017.

Muro amesema, Klabu ya Soka ya Yanga itapinga usajili wa mchezaji huyo kwa klabu yoyote itakayotaka kumsajili bila ya kulipa gharama anazotakiwa kuilipa Klabu hiyo, hivyo kama kuna timu itamuhitaji itabidi kulipa kwanza kiasi hicho ndipo Klabu ya Yanga itaridhia mchezaji huyo kuendelea na klabu nyingine yoyote.

Uamuzi huo umefikiwa na kikao cha kamati ya nidhamu ya klabu, baada ya kulichunguza kwa umakini suala la mchezaji huyo na historia yake ya nidhamu pia ndani ya klabu tangu asajiliwe miaka minne iliyopita.

Sakata la sasa la Niyonzima linaanzia mwezi uliopita baada ya mchezaji huyo kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini Ethiopia na akachelewa kurejea baada ya mashindano.

Kufuatia hali hiyo, klabu ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye imekuja na maamuzi magumu.

Pamoja na Niyonzima kuwasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu ulijiaminisha kiungo huyo amedanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.

Uongozi ulidai kuwa ulibaini plasta ngumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.

Kwa upande mwingine, Niyonzima amesema hana taarifa za Klabu hiyo kuvunja naye mkataba kwani hajapokea barua yoyote kutoka klabuni hapo.